Shirika la ELimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa UNESCO limesema mauaji ya Waandishi wa Habari na wafanyakazi katika vyombo vya Habari yaliongezeka kutoka 55 hadi 86 kote ulimwenguni, ikiwa ni tukio la kifo cha mtu mmoja katika kila siku nne.
Mkurugenzi mtendaji wa UNESCO, Audrey Azoulay amesema miongoni mwa Wanahabari waliouwa, matukio 19 yaliripotiwa nchini Mexico, 10 Ukraine na tisa nchini Haiti na kudai kuwa ongezeko la idadi ya wanahabari waliouawa mwaka 2022 linaleta wasiwasi.
UNESCO, pia ilibaini kuwa hakuna yeyote aliyewajibishwa katika asilimia 86 ya visa hivyo huku Ripoti hiyo ikitaja dhuluma nyingine dhidi ya waandishi wa habari ikiwemo kutoweka, kutekwa nyara, kukamatwa kiholela, kuhangaishwa kisheria na kushambuliwa.
Kufuatia matukio hayo, Azoulay ametoa wito kwa Mataifa na Serikali kuongeza juhudi za kukomesha dhuluma dhidi ya Wanahabari ikiwemo kuimarisha sheria zinazowalinda na wahusika wanaoshiriki matukio ya udhalimu dhidi yao wachukuliwe hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.