Mwanaharakati wa hali ya hewa Jean Claude Brou amesikitishwa na kutokuwepo kwa mashahidi wa athari za uharibifu wa ardhi na mazingira katika mkutano wa umoja wa mataifa wa kupambana na kuenea kwa Jangwa (UNCCD).

Mkutano huo wa COP15 uliofanyika jijini Abidjan nchini Ivory Coast umefikia tamati Mei 20, 2022 kwa maamuzi 38 ikiwepo kurejesha ardhi na kupunguza ukame ambapo Brou amesema kutowaalika wakulima kunafanya mkutano kukosa maana.

“Wakulima ndio wanaofahamu hali halisi ya uharibifu wa ardhi na wao wanapambana na hali hii kila siku wao wanajua ukweli wote na wanajua uhalisia wa misitu lakini hapa hawapo sisi tunafanya nini,” amelalama Brou.

Amesema ni vyema wakati mwingine kuweka utaratibu wa kuwaalika wakulima katika mikutano ya mambo yanayohusu ardhi badala ya kuita watawala, kamati au mashirika ya kilimo kuhudhuria ambayo hayajui uhalisia wa uharibifu.

Katika mkutano huo baadhi ya wajumbe wamesema asilimia 40 ya uso wa dunia tayari imeharibiwa kwa shughuli za binadamu na kudai bila ya kuchukua hatua madhubuti hali inaweza kuwa mbaya zaidi.

“Kiukweli natoa mwito wa kuchukua hatua katika masuala makuu mawili marejesho ya ardhi na kuukabili ukame la sivyo uso wa dunia utazidi kuharibika,” amesema mjumbe  kutoka nchi ya Mauritania.

Ingawa ukame ni suala la kimataifa ripoti ya hivi karibuni ya Umoja wa Mataifa imebainisha kuwa bara la Afrika ndilo lililoathiriwa zaidi likifuatiwa na lile la Amerika, India na Australia.

Hali hii imefanya vyama 196 kuahidi katika mkutano huo kuongeza uwezo wa kustahimili ukame na kuwekeza katika kurejesha ardhi kwa ajili ya ustawi wa siku zijazo.

Ufuatiliaji wa takwimu na maendeleo ya ahadi za kurejesha ardhi ni moja ya maazimio 38 ya mkutano huo na kwamba uwepo wa msukumo mpya na uwezo wa kifedha utasaidia mataifa kukabiliana na athari husika.

Jumla ya Dola za Kimarekani bilioni 2.5 zimetajwa kuhitajika kusaidia mpango wa kukabiliana na ukataji wa miti na mabadiliko ya hali ya hewa.

Kilele cha mkutano huo wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa kitafanyika nchini Misri mapema mwezi Novemba 2022.

Habari Kuu katika magazeti ya leo Mei 22, 2022 
Wahariri chanzo ukuaji wa biashara