Wahariri wa vyombo vya habari wametajwa kuwa na nafasi kubwa ya kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara nchini kwa kutumia vyombo na Taaluma zao.

Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji ameyasema hayo hii leo Mei 21, 2022 kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Hashil Abdallah katika kikao kazi cha siku mbili kati ya wahariri wa vyombo vya habari na Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA), kinachoendelea Mjini Morogoro.

“Wahariri naomba tushirikiane kwa pamoja kufanikisha ukuaji wa sekta ya biashara na wananchi warasimishe biashara zao na kupitia nyie watakuwa na uelewa wa mambo mengi,” amesema Dkt. Abdalah.

Amesema kupitia kikao kazi hicho anaamini wahariri watakuwa mabalozi wazuri wa BRELA kwa kuzibeba ajenda za wakala huo hasa kwenye eneo la urasimishaji wa biashara ili wananchi waweze kupata taarifa zitakazowanufaisha.

“Lakini pamoja na hilo BRELA mnapaswa kuendelea kuimarisha ushirikiano na vyombo vyote vya habari na kila mnapotakiwa kutoa ufafanuzi wa jambo fulani msisite kufanya kwani wahariri huandika habari kwa usawa na hii itasaidia sana katika uelimishaji,” ameongeza Dkt. Abdallah.

Hata hivyo Dkt. Abdalah amewaomba wahariri wa vyombo vya Habari kutumia lugha rahisi na ya kueleweka kwa wananchi pindi wanapoandika taarifa za BRELA kwani mambo mengi ya wakala huo yapo kisheria.

“Wahariri wengine wanaweza kuwa na mitazamo tofauti kwa namna wanavyotafsiri sheria za utekelezaji wa majukumu ya BRELA na hii inaweza kupelekea uandishi wa kichwa cha habari kinachohukumu na kuleta taharuki kwa umma,”amefafanua Dkt. Abdalah.

Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni Godfrey Nyaisa amesema usimamiaji wa majukumu ya msingi ya BRELA umewezesha kuwa na mafanikio yenye uwazi na ukuaji wa uchumi wa Tanzania.

Uboreshaji wa mazingira ya biashara na urahisishaji wa sajili na leseni zinazotolewa na BRELA hapa nchini utokana na utekelezaji wa mikakati mikuu ya sera na mpango wa Maendeleo ya Taifa.

Mwanaharakati ang'aka kukosekana wakulima UNCCD
Mbatia afungiwa mlango Nyumbani kwake