Rais wa Zanzibar na Mwenyikiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi, amesema kutokana na juhudi za serikali kutimiza lengo la Elimu bila malipo, idadi ya skuli imeongezeka kufikia 153 kutoka skuli moja kabla ya mapinduzi, msingi 577 na sekondari 228 kutoka tano kabla ya mapinduzi ya mwaka 1964.
Dkt. Mwinyi ameyasema hayo kupitia hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Masoud Othman katika Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar wakati wa maadhimisho ya kilele cha Tamasha la kutimia miaka 58 ya Elimu bila malipo Zanzibar.
Amesema, maendeleo makubwa yamepatikana katika Sekta ya Elimu nchini tangu kutangazwa elimu bila malipo miaka 58 ilyopita, yakitokana na matokeo ya juhudi za Serikali katika utekelezaji wa mkakati wake wa kuimarisha miundombinu ya upatikanaji wa huduma hiyo ikiwemo ujenzi wa taasisi za elimu za ngazi mbali mbali.
Akizungunzia Vyuo Vikuu, amesema kabla ya Mapinduzi Zanzibar haikua na chuo Kikuu hata kimoja, lakini hivi sasa vipo vinne vyenye jumla ya
wanafunzi 12,527 na pia ipo taasisi ya ufundi Karume na vipo vyuo vitano vya mafunzo ya amali na vituo vya Elimu mbadala Unguja na Pemba.
Ameoengeza kuwa, shabaha ya serikali ni kutatua changamoto zote zilizopo katika sekta hiyo kwa kuongeza miundombinu ya kujifunzia na kufundishia, ili kufikia azma ya serikali ya kuwa na wasomi wakaoweza kuongeza idadi ya wataalamu kila fani ili kusaidia ujenzi wa nchi.
Kuhusu maslahi ya waalimu, Mwinyi amesema Serikali imepandisha mishahara ya walimu kuahidi kwamba Serikali itaendelea kuangalia maslahi ya wafanyakazi hao kadri uwezo wa uchumi unavyoruhusu.
Hata hivyo, amesema hatua hiyo imepelekea kuongeza fursa za upatikanaji wa elimu kwa watoto katika ngazi mbali mbali bila ya ubaguzi wa aina yoyote sambamba na kuongezeka ujenzi wa wa taasisi za elimu kama dhamira ya mapinduzi ya mwaka 1964 ya kuweka fursa sawa ya elimu kwa wote.
Aidha, Rais Mwinyi amesema Serikali inaendelea kufidia michango ya elimu iliyokuwa ikitolewa na wazazi na wanafunzi wote wa skuli za Serikali za maandalizi hadi sekondari wanaendelea kupatiwa elimu bila kulipa na serikali ikizipatia skuli nyenzo na vitendea kazi kama vile chaki na madaftari.
Awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Maunzo ya Elimu, Ali Khamis Juma amsema kwamba katika jitihada za serikali kuendelea kuimarisha sekta ya elimu na kufanya mageuzi katika sekta hiyo imeunda kikosi kazi na tayari kinafanya kazi kubwa ya kupokea maoni ya wadau kuhudu haja ya mabadiliko katika elimu Zanzibar.