Kwa mujibu wa tafiti zilizofanywa na Taasisi za kimataifa, Tanzania inashika nafasi ya sita kwa Bara la Afrika kwa kuwa na gharama za chini za vifurushi vya simu ”bando” ambapo kwa Duniani inashika nafasi ya 32 kuwa na gharama za chini za data.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye wakati akitoa ufafanuzi juu ya suala hilo kupitia kituo kimoja cha Habari jijini Dar es Salaam Agosti 20, 2022 na kusema bei ya data kwa wastani wa 1GB ni Dola 1.71 sawa na shilingi 3990.

Amesema, “Tanzania kuwa miongoni mwa Mataifa yenye gharama za chini za mawasiliano haimaanishi kuwa itapunguza malalamiko kwa kuwa uchumi wetu haufanani na wananchi wengi wana kipato cha chini.”

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye.

Nape ameongeza kuwa, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), inaendelea kufanya tathmini ya gharama za uwekezaji, utunzaji na usafirishaji wa data kila baada ya miaka minne na tathmini nyingine inafanyika mwaka huu ili kupata uhalisia wa gharama za bando.

Ameongeza kuwa, “Wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa Serikali yao ni sikivu na inafanyia kazi malalamiko na maoni yao, lakini pia nitoe rai kwa wananchi kuwa makini na matumizi ya simu janja hasa kwenye kujiunga na huduma ili kupunguza matumizi ya bando.”

Hata hivyo, Nape amesema Serikali imeruhusu ushindani kwa kuweka mazingira wezeshi ya kuwa na kampuni nyingi zinazotoa huduma za mawasiliano, ambapo suala la vifurushi ni huduma ya ziada inayotolewa na makampuni hayo.

Serikali kuwapatia eneo Wachimbaji wadogo utafiti wa Madini
Kenya: Odinga awaambia Viongozi wa Dini ana ushahidi wa kutosha