Rais Dkt. John Pombe Magufuli amepongezwa kwa moyo wake wa kujitoa na kuwajali wanyonge hasa wagonjwa wasiojiweza na wenye uhitaji  wa gharama za matibabu.

Hayo yamesemwa leo na Neema Mwita Wambura maarufu kama ‘Mgonjwa wa Magufuli’ wakati alipotembelewa na waandishi wa habari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es salaam ambako alilazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu baada ya kupata majeraha ya moto.

“Ninamshukuru sana Rais Dkt. Magufuli kwa msaada wake katika matibabu yangu. Hivi sasa mimi nina maendeleo makubwa, naweza kuongea, kula na hata kugeuza shingo yangu. Nitamuombea Rais Magufuli mpaka siku naingia kaburini, Mungu ambariki” amesema Neema.

Aidha, akisimulia kile kilichompata, Neema amesema kuwa alimwagiwa maji ya moto na mumewe baada ya kuchuma mahindi mawili (2) shambani bila ya ruhusa yake. Mumewe huyo alitoweka na ndugu za Neema walihofia kumchukua kwa kuogopa kudaiwa mahali iliyolipwa na mumewe kama taratibu za kumuoa.

Katika matatizo yaliyompata, Neema amesema kuwa hakuna ndugu yake hata mmoja aliyejitokeza kumsaidia kipindi chote cha matibabu na kusema kuwa walikuwa wakihofu kuwa angeweza kufariki na mahali zote alizolipiwa zingeweza kurudishwa, amesema kuwa tayari alikuwa ameshakata tamaa na alichokuwa akisubiri ni siku yake ya kufariki ifike.

Pia, Neema amewashukuru watumishi wa Hospitali ya Taifa Muhimbili wodi ya Mwaisela wakiwemo manesi na madaktari kwa upendo na msaada mkubwa waliompatia toka siku walipompokea katika hospitali hiyo mpaka sasa ambapo anatarajia kurudi nyumbani.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Upasuaji ambaye pia ni Daktari bingwa wa upasuaji Dkt. Ibrahimu Mkoma amesema kuwa, Neema alipokelewa hospitalini hapo tarehe 06/07/2015 akitokea Mkoa wa Mara wilaya ya Musoma , Neema alikuwa na majeraha ya mwaka mmoja toka aunguzwe.

Mpaka sasa Neema ameshafanyiwa oparesheni tatu kwa nyakati tofauti, zilizohusisha kutengenisha baadhi ya viungo kwani shingo, kifua na mkono wa kushoto vilishikana, ambapo ilibidi kutoa ngozi ya sehemu ya mwili ili kufunika sehemu zile zilizoathirika zaidi.

Hata hivyo, Dkt. Mkama ametoa wito kwa wadau na taasisi zinazohusika katika kutoa elimu kwa umma hususan madhara ya vitendo vya kikatili kutoa elimu hiyo kwa kuzingatia sehemu zenye ukubwa wa tatizo hilo ili kumaliza kabisa majanga ya aina hiyo.

Video: Wauza Nyama Dar Walia Bei Kushuka
Ndege yaanguka na kuua watano, yadaiwa kuna ‘manusura’