Mwanamke mmoja aitwaye Rebecca Siowi (30) mkazi wa Kilimanjaro amemzika mtoto wake nyuma ya nyumba usiku wa kuamkia Aprili 22, 2022 nyumbani kwa bibi yake walikokuwa wakiishi yeye pamoja na mama yake baada ya mume kumtelekeza na watoto watano.

Mtoto huyo aliyejulikana kama Salah Jackson (5) mwenye ulemavu wa viungo, mkazi wa kijiji cha Makiwaru, mkoani Kilimanjaro alifariki dunia kutokana na njaa na kisha mama yake mzazi kumzika kimya kimya usiku wa manane.

Tukio hilo liligundulika baada ya mtoto huyo kutoonekana jioni ya Aprili 21 nyumbani, ambapo bibi yake huyo alifanya jitihada za kumtafuta bila mafanikio ndipo Aprili 22 alipobainika kuwa amezikwa.

Kamanda wa polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amekiri kuwepo kwa tukio hilo, na kusema baada ya kupata taarifa ya tukio hilo kutoka kwa wananchi walifika eneo la tukio kuona sehemu alipozikwa mtoto huyo na walilazimika kuomba kibali cha kuufukua mwili wa mtoto huyo ili kujua sasababu za kifo cha chake.

“Hili tukio kweli lipo na baada ya Jeshi la polisi kupata taarifa juu ya tukio hilo tulienda kuomba kibali cha kufukua mwili wa mtoto ili kujiridhisha sababu za kifo cha mtoto huyo ni nini kutokana na maneno mengi yaliyokuwepo mtaani.

“Tulifukua mwili jana na kuupeleka hospitali kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na majibu ya daktari yalipotoka yalionyesha kwamba huyu mtoto alikufa kutokana na njaa,” amesema Kamanda Maigwa.

Akizungumzia tukio hilo, jirani wa familia hiyo, Maria Nko amesema hata kama mtoto huyo alikufa kwa njaa mama yake huyo hakupaswa kumzika mwanaye kama mbwa tena usiku wa manane.

“Kwa kweli hili tukio linaumiza na inaonekana huyu mama alikuwa akimtesa huyu mtoto kutokana na ulemavu aliokuwa nao, inakuwaje hao watoto wake wengine hawajafa na njaa na kwa nini amzike mwenyewe tena?” amehoji.

Congo yarekodi kisa kipya cha ebola
Waziri Gwajima azuru Kaburi la Mtoto aliyeuwawa na bibi yake