Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi limefanikiwa kuwakamata na kuwafikisha Mahakamani watuhumiwa 121 waliohusishwa na matukio mbalimbali ikiwemo wizi na unyanganyi wa kutumia silaha mkoani humo.
Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Desemba 5, 2023 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, ACP Kaster Ngonyani amesema watuhumiwa wote wamekatwa kwa kipindi cha mwezi mmoja uliopita.
Kamanda Ngonyani amesema kati ya watuhumiwa hao 121, watuhumiwa 77 wamehusishwa na matukio ya wizi, unyang’anyi, uporaji na uvunjaji huku akibainisha kuwa walikamatwa na vielelezo na mali mbalimbali za wizi.
Watuhumiwa wengine saba walikamatwa na nyara za Serikali meno matatu ya mnyama adhaniwaye ni Tembo na vipande kumi vya nyama pori aina ya Nyati na Kongoni, watuhumiwa 17 wamekatwa na Pombe ya moshi (Gongo), kiasi cha lita 135 na mtambo mmoja wa kutengenezea pombe hiyo na watuhumiwa watatu wakikamatwa na dawa za kulevya zidhaniwazo kuwa ni bangi kete 13.
Katika hatua hatua nyingine ACP Ngonyani amesema Jeshi la Polisi linawashikilia watuhumiwa wawili waliotuhumiwa kujihusisha na wizi wa Ng’ombe.
Amesema jumla ya watuhumiwa 112 wamefikishwa Mahakamani ambapo watuhumiwa 49 wamehukumiwa vifungo, 25 kulipa faini, watatu wameachiwa huru na watuhumiwa 35 bado kesi zao zinaendelea Mahakamani.