Wiki iliyopita Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alitoa habari iliyotarajiwa kuwa ‘njema sana’ kwa walimu wote wa shule za msingi na sekondari jijini Dar es Salaam, kupata upendeleo wa kupunguza makali ya gharama za maisha kwa kupanda usafiri wa umma maarufu kama daladala ‘BURE’ kila waendapo na kutoka kazini.

Paul Makonda

Msaada huo una thamani ya kati ya shilingi 800 hadi shilingi 1,500 kwa siku kwa mwalimu mmoja atakayepanda daladala jijini Dar es Salaam wakati wa kwenda na kutoka kazini.

Hata hivyo, habari hiyo iliyopakuliwa mithili ya asali mbichi kutoka kwenye mzinga kwa ajili ya wapewa walimu wenye mchango mkubwa kwenye taifa hili, iligeuka kuwa shubiri kwenye bakuli walilotengewa.

Wengi, na naamini hasa timu nzima ya Paul Makonda pamoja na wadau wa elimu waliojitoa kutoa msaada huo ‘adhimu’ hawakutegemea kama walengwa wangepiga teke kile kilichodhaniwa kuwa ni ‘bakuli la dhahabu’, kwa kuzingatia ukweli kuwa ni askari wa majeshi yetu pekee ambao ndio wafanyakazi wa umma wanaopanda daladala ‘BURE’ nchi nzima ili mradi wawe ndani ya sare zao za kazi.

Lakini hali ilikuwa tofauti baada ya Chama Cha Walimu nchini (CWT) pamoja na baadhi ya walimu kupinga kwa nguvu msaada huo wakimtaka Mkuu huyo wa Wilaya kuacha kile walichokiita ‘kuwadhalilisha’ huku wakiibua matatizo mengine ya muda mrefu ambayo ni dhahiri kwamba hayakuwa jukumu la Paul Makonda ambaye ni muwakilishi tu wa Rais katika wilaya yake ya Kinondoni pekee, na zaidi ya hapo ni mdau wa elimu… niweke ‘fulu stopu’.

Kwa mantiki hiyo, ni dhahiri kuwa kilichotokea ni sawa na Makonda kuwatonesha walimu hao kidonda kwa msaada ambao wao waliona sio jambo la msingi kwao.

Shule ya msingi Kanawa kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga (2015)

Shule ya msingi Kanawa kijiji cha Negezi kata ya Ukenyenge wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga (Machi 2015)

Baadhi ya walimu wamedai kuwa watakuwa wanadhalilishwa kuonesha vitambulisho ili wapande bure daladala huku wanafunzi wakilipa shilingi 200.

Wengine walienda mbali na kukejeli kuwa huenda wakalazimika kuwapisha wanafunzi ‘seat’ kwakuwa wao watakuwa wanajulikana ‘wapanda bure’, kwahiyo madereva na makondakta wataona bora wanafunzi wanaolipa.

Mwalimu mmoja mzoefu sana na aliyehitimu chuo kikuu katika fani hiyo, Aristotle Kirigha, alimuandikia Paul Makonda Barua ya wazi kwenye ukurasa wake wa Facebook akimuorodheshea mambo ambayo anaamini Makonda alipaswa kuishauri serikali kuwa ndicho kipaumbele cha walimu na sio kupanda bure usafiri wa daladala.

“Kwa uelewa wangu, matatizo ya Walimu ni haya:
1. mishahara midogo
2. hakuna allowance
3. hakuna nyumba
4. bima isiyokidhi haja
5. Ucheleweshaji wa stahiki kama madaraja, mapunjo, fedha ya likizo nk.
6. Mazingira magumu ya Kazi kama vijijini.
7. Fedha za likizo n.k.
Halafu yale ya msingi kabisa, yanayokera (the most pressing teachers problem) ambazo MTU mwenye nia anatakiwa kudeal nayo ni haya:
1. Nyongeza ya mishahara (salary scale)
2. Kupewa allowance
3. Nyumba
4. Kupewa stahiki kwa wakati.

Maswali yangu ni haya:
1. Hivi P. Makonda anafahamu matatizo haya?
2. Je, walimu wa Dar, waliomba kupanda basi bure?
3. Je hili ni ombi la CWT?
Makonda na walimu wake wa Kinondini hawakuangalia upande wa pili. Kwa sababu,
1. Wanafunzi wamedhalilishwa sana na makondactor kwa nauli yao ndogo wakaitwa mawe.”

Je, walimu wataitwa jina gani? Mi nadhani sasa ndo walimu watachelewa zaidi kazini kwa kuachwa kwenye vituoni.

Hata hivyo, Paul Makonda ameyatolea majibu maswali na hoja za wanaopinga msaada huo huku akisisitiza kuwa wanamtukana wanamuongezea nguvu ya kufanya kazi zaidi.

Makonda anataka walimu waelewe kuwa matatizo yao na Serikali ni tofauti na msaada huu uliotolewa na wadau wa elimu kwa moyo wao, na sio serikali.

“Hii sio serikali ni wadau, serikali imetumika kama daraja. Wasichanganye mambo… ni wadau wanasaidia sekta ya elimu. Ni kama vile tunavyopokea mifuko ya cement, huwezi kumwambia anayekuletea cement mimi nataka mbao hizi sizitaki!,”alisema Makonda.

“Chama cha Walimu wangesema, yakwamba tumepokea nafasi ambayo jamii sasa imeanza kutambua heshima ya walimu katika Taifa, kwa moyo huu huu ambao wadau wameendelea kuuonesha tunaendelea kuiomba Wizara ya elimu iendelee kuboresha zaidi,” aliongeza.

Mimi naamini huu ni msaada uliotolewa kwa nia njema na ya dhati lakini bahati mbaya umegeuka kuwa chunvi kwenye kidonda kibichi cha walimu ambao bado ndio watumishi wa umma ambao wanachangamoto nyingi za ujira huenda kuliko kada nyingine.

Walimu wanatamani siku moja kazi yao isiitwe ‘kazi ya wito’ bali iwe kazi ya heshima kubwa na kukimbiliwa kama ilivyo kwa kazi nyingine za umma, ukizingatia mchango wao mkubwa kwa Taifa.

SAMATTA AZIDI KUPAA, ATINGA 'GAME YA FIFA'
Gloves zawatumbua majipu wauguzi