Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) Mkoa wa Temeke imetaja Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Mahakama, Polisi na Sekta Binafsi kuongoza kwa kulalamikiwa zaidi kwa vitendo vya rushwa dhidi ya wananchi ambapo jumla ya taarifa na malalamiko 232 ziliwasilishwa kwao.
Hayo yamesemwa jijini Dar es salaam na Mkuu wa Takukuru wilaya ya Temeke, Pilly Mwakasege ambapo amesema kuwa taarifa hizo ni za kipindi cha mwezi Oktoba mwaka 2017 hadi Machi 2018 ambapo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke imekuwa na malalamiko 87, Mahakama 37 na malalamiko 26 ni ya Jeshi la Polisi ambapo malalamiko yote yameshughulikiwa na kesi kupelekwa Mahakamani.
Amesema kuwa Takukuru imeweza kuokoa zaidi ya shilingi milioni 44 kutoka kwenye mishahara hewa, mfuko wa jimbo, malipo ya zabuni kwani wanasimamia fedha zote za miradi ya maendeleo na kuwahimiza wananchi kuendeleza ushirikiano na mamlaka hiyo katika kudhibiti vitendo vya rushwa.
Hata hivyo, Mwakasege ameongeza kuwa wanaendelea kutoa elimu kwa umma kwa lego la kuwa elimisha wananchi Juu ya Haki na Wajibu wao katika kupambana na rushwa, kuwa elewesha njia za kuwasilisha malalamiko na kutoa elimu ya uelewa wa masuala ya rushwa.