Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba amemtaka Rais John Magufuli kutangaza mshahara wake pamoja na posho zake ili kuvunja utata ulioachwa na watangulizi wake na kuendana na dhana ya kuwa Rais wa Wanyonge.

Profesa Lipumba ameeleza kuwa Rais Magufuli anapaswa kuchukua hatua hiyo kutokana na namna anavyojipambanua kwa wananchi kuwa yeye ni Rais wa wanyonge na kwamba atumie sehemu ya mshahara wake au malupulupu yake katika kusaidia jamii.

Mwanasiasa huyo alitumia takwimu zilizowahi kutokelewa na baadhi ya vyombo vya habari  na baadae kukanushwa na Ikulu, zilizodai kuwa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete alikuwa akipokea mshahara wa shilingi milioni 32 kila mwezi.

“Kwa hivi sasa Rais Magufuli atangaze mshahara na marupurupu yake na kama mapato yake ni Sh32 milioni kwa mwezi, basi ajitolee alau nusu ya mapato hayo kuchangia elimu na afya ya wanyonge. Hatua hii itaimarisha taswira inayojengeka barani Afrika kuwa yeye ni Rais wa wanyonge,” Lipumba ananukuliwa na gazeti la Mwananchi lilofanya  naye mahojiano maalum.

Alieleza kuwa Rais anapaswa kujitolewa mchango wa kudumu kwa jamii kutoka kwenye mshahara wake hususan katika kusaidia sekta ya Afya na elimu.

Mwanasiasa huyo mkongwe ambaye pia ni mtaalam masuala ya kiuchumi na mshauri wa Benki Kuu ya Tanzania katika masuala ya Kiuchumi, alizitaka Mamlaka husika kuweka taratibu za mfumo ulio wazi wa kuamua mishahara ya Rais, Makamu wa Rais, Wabunge, Majaji na Mawaziri.

Alieleza kuwa kutoka na taarifa za posho waliyokuwa wanalipwa wabunge, kikao cha siku moja tu ambazo ni shilingi 330,000 ni mara mbili ya mshahara wa kima cha chini ambacho ni shilingi 150,000.

Chanzo: Mwananchi

Timu ya Donald Trump yaendelea kumshambulia Papa Francis, yaja na zito zaidi
Magufuli afanya ziara ya kimyakimya kivukoni