Jeshi la Polisi Nchini limepatiwa elimu ya mafao toka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kwa lengo la kuimarisha uhusiano wa kiutendaji baina ya taasisi hizo katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja.
Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini wa Jeshi hilo Naibu Kamishna wa Polisi, DCP Gabriel Semiono kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi amesema elimu hiyo itasaidia Askari wa Jeshi hilo kupata uelewa wa pamoja kuhusiana na mabadaliko ya sheria mbalimbali za uendeshaji wa mifuko ya Kijamii.
DCP Semiono amebainisha kuwa kupitia elimu hiyo ambayo wataipata wataenda kutatua kero pamoja na changamoto mbalimbali ambazo Askari wanakumbana nazo wakati wakifuatilia stahiki zao za mafao hususani pindi wanapostaafu kazi.
Aidha, amewataka washiriki wote kufuatilia kwa makini mada zote zitakazotolewa lakini pia kutoa maoni na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika utendaji wao wa kazi, huku Mkurugenzi wa Uendeshaji katika Mfuko huo, Mbaruku Magawa akisema lengo la kikao hicho ni kutoa elimu na kupokea mrejesho wa huduma wanazozitoa kwa jeshi hilo.
Amesema, baada ya semina hiyo anaamini kutakua na mabadiliko makubwa katika utendaji wa kazi hususani katika kutoa huduma bora kwa wateja, ambapo kikao hicho kilichoanza hii leo Juni 5, 2023 kinatarajia kufikia tamati hapo kesho Juni 6, 2023.