Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Msajili wa Vyama vya Siasa Jaji Francis Mutungi, kuitisha kikao maalum cha Baraza la Vyama vya Siasa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa hii leo imeeleza kuwa lengo la kikao hicho ni kuwashirikisha wadau katika kutathmini utekelezaji wa
mapendekezo ya Kikosi Kazi kilichokuwa kikiratibu maoni ya watu kuhusu demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini.
Rais Samia ametoa maelekezo hayo wakati wa kikao kilichofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma, kilichohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali kikihusu kuanza kwa mchakato wa Katiba mpya.
Kikao hicho kimejadili namna ya kushirikisha wadau mbalimbali na hasa ushirikishwaji wa wananchi katika mchakato huo kutoka pande zote mbili za Tanzania Bara na Zanzibar.
Mbali na mchakato huo wa Katiba mpya, masuala mengine yanayotarajiwa kushughulikiwa ni marekebisho ya sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi zikiwemo Sheria ya Tume ya Uchaguzi, Sheria ya Vyama vya Siasa
na Sheria ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Miongoni mwa viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenista Mhagama, Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Damas Ndumbaro na watendaji wa taasisi mbalimbali.