Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amewataka viongozi wa umma kushughulikia kero na changamoto wanazowasilishiwa na mfumo wa Sema Na Rais (SNR).
Rais Dk.Mwinyi ameyasema hayo hii leo Machi 29, 2023 kwenye kikao kazi cha maadhimisho ya miaka miwili tangu kitengo cha Sema na Rais Mwinyi (SNR), kilipoasisiwa ambacho kipo chini ya Afisi ya Rais Ikulu.
Amesema, wapo baadhi ya viongozi wasiotaka kutatua changamoto hizo na kwamba atawachukulia hatua, huku akibainisha kupitia mfumo huo kuna utambuzi wa kitakwimu kujua kiongozi au taasisi zisizofanya vizuri na hivyo wakati umefika wa kuona umuhimu wa uwajibikaji.
Akizungumzia mafanikio ya mfumo wa SNR kwa kipindi cha miaka miwili, Dkt. Mwinyi amesema umeleta tija kwa wananchi, kwa changamoto zao kutatuliwa kwa kiasi kikubwa na mfumo ataendelea kuusimamia vema.
Kuhusu suala la taarifa za ubadhirifu wa mali za umma na akaonya asitokee Kiongozi yeyote kuwatisha wanaowasilisha kero au changamoto kupitia mfumo wa SNR na akaahidi hatua zitachukuliwa dhidi ya kiongozi huyo. Ameahidi mtoa taarifa atalindwa na kuwaambia maafisa wa SNR wafanye kazi zao bila woga.