Kongamano la Nishati Safi ya Kupikia, litafanyika Novemba 1-2, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dares Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, likiwa na dhima ya kufahamu hali ya sasa ilivyo nchini na kutafuta uelewa wa pamoja wa wadau kwa kubadilishana ujuzi, uzoefu, na fursa zitakazowezesha kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati bora ya kupikia.
Hayo, yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba hii leo Oktoba 12, 2022 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa Habari na kusema asilimia 90 ya nishati yote inayotumika majumbani ni tungamotaka (Biomas), yaani kuni na mkaa, ambapo asilimia 63.5 ya kaya zote nchini zikitumia kuni kupika na asilimia 26.2 wakitumia mkaa na kaya zinazotumia gesi ya mitungi (LPG), kupikia ni asilimia 5.1, asilimia 3 umeme na asilimia 2.2 vyanzo vingine.
Amesema, kongamano hilo pia litapitia na kujadili sera, sheria pamoja na mikakati ya kifedha na kiteknolojia itakayosaidia kutatua changamoto Zinazokwamisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kila nyumba, kutafuta namna bora ya kufikia malengo ya nishati safi ya kupikia kwa wote, na kuongeza fursa za ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja katika masula ya nishati safi ya kupikia.
Aidha, pia litahusisha mada za majopo matano yatakayojadili na kuzungumzia, (i). Upatikanaji na kuweza kumudu mbadala wa Biomasi (kuni na mikaa), (ii). Je, tunaweza kupeleka gesi ya kupikia nyumbani (LPG) kwa wananchi? (iii). Nishati ya Kupikia na Ustawi wa Wanawake, (iv). Ugharimiaji wa Nishati Safi ya Kupikia (v). Mtazamo wa afya kwenye matumizi ya nishati ya kupikia.