Serikali nchini, imesema asilimia 72 ya nishati yote inayozalishwa nchini Tanzania inatumika majumbani na ni asilimia 8 pekee ya Watanzania ndio wanaotumia nishati safi ya kupikia na waliobakia wamekuwa katika hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukizwa kutokana na kuvuta moshi utokanao na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia.

Hayo, yamebainishwa na Waziri wa Nishati, Januari Makamba hii leo Oktoba 12, 2022 jijini Dar es Salaam katika mkutano na waandishi wa Habari na kusema tatizo hilo pia linahusisha watu wa nyanja tofauti za wenye kipato na wasio na kipato hasa katika maeneo ya Vijijini.

Amesema, “Asilimia 90 ya nishati yote inayotumika majumbani ni tungamotaka (Biomas) yaani kuni
na mkaa, asilimia 63.5 ya kaya zote nchini zikitumia kuni kupika na asilimia 26.2 wakitumia mkaa na kaya zinazotumia gesi ya mitungi (LPG), kupikia ni asilimia 5.1, asilimia 3 umeme na asilimia 2.2 vyanzo vingine.”

Waziri Makamba amebainisha kuwa, athari zitokanazo na matumizi ya nishati isiyo safi ya kupikia hupelekea mzigo kwenye mfumo wa utolewaji wa huduma za afya nchini na kusababisha vifo vya watu 33,000 kutokana magonjwa ya mfumo wa upumuaji huku Wanawake na watoto wakitumia muda mwingi kutafuta kuni, nafasi ambayo wangeweza kuitumia kwenye shughuli za maendeleo.

Aidha amesema, kutokana na hali hiyo Wizara imepanga kuchukua hatua za kuwasaidia wananchi juu ya kupata nishati safi ya kupikia, ili kuongeza ustawi wa kiafya kwa watanzania kwani tatizo la magonjwa yatokanayo na moshi wa nishati isiyo safi ya kupikia, limeendelea kuwaathiri watu wengi hasa akina mama.

Amesema, “Matumizi ya nishati isiyo safi au yale ya kutumia kuni husababisha madhara kwa mwili wa binadamu kutokana na moshi ambao umekuwa na sumu na kama mnaelewa mbegu za mahindi kijijini huhifadhiwa na wakulima jikoni sasa pale moshi hufanya ziwe nyeusi na wadudu hawawezi kula maana ile ni sumu.”

Baadhi ya Waandishi wa Habari wakimsikiliza Waziri Makamba jijini Dar es Salaam hii leo Oktoba 12, 2022.

Ameongeza kuwa, athari za mazingira kutokana na uchafuzi wa hali ya hewa ikiwemo mabadiliko ya tabia
nchi vimepelekea vitendo vya ukatili wa kijinsia kama kubakwa au kupigwa kwa wanawake na watoto wanaotumia muda mwingi kutafuta kuni kitu ambacho kimeifanya Serikali Kuanzisha mjadala wa kitaifa kuhusu nishati safi ya kupikia kwa minajili ya kutambua na kutatua changamoto hiyo hasa wanawake na watoto waliopo vijijini na kuwasaidia kupaza sauti juu ya matukio yasiyofaa didi yao.

Aidha, Waziri Makamba ameongeza kuwa, ili kuweza kufanikisha mpango huo Serikali itaangalia mifumo ya kiutawala, kikodi, kisheria na kisera, hatimaye kuongoza thamani nishati safi ya kupikia na kwamba
Sera ya Taifa ya Nishati (NEP), ya mwaka 2015 itasaidia kuwezesha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia yenye gharama nafuu na ya uhakika.

“Kwa mwaka wa fedha 2022/23, Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), imetenga shilingi milioni 500 ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia, lengo namba 7 la Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDG 7) linataka kila nchi kuhakikisha upatikanaji wa nishati bora na ya kisasa kwa wote kwa bei nafuu, kwa uhakika na njia endelevu.” amefafanua Waziri Mkamba.

Kongamano hilo la Nishati Safi ya Kupikia, litafanyika Novemba 1-2, 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dares Salaam na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, likiwa na dhima ya kufahamu hali ya sasa ilivyo nchini na kutafuta uelewa wa pamoja kwa wadau wote kwa kubadilishana ujuzi, uzoefu, na fursa zitakazowezesha kutatua changamoto za upatikanaji wa nishati bora ya kupikia.

Kongamano hilo pia litapitia na kujadili sera, sheria pamoja na mikakati ya kifedha na kiteknolojia itakayosaidia kutatua changamoto Zinazokwamisha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa kila nyumba, kutafuta namna bora ya kufikia malengo ya nishati safi ya kupikia kwa wote, na kuongeza fursa za ushirikiano na kufanya kazi kwa pamoja katika masula ya nishati safi ya kupikia.

Aidha, pia litahusisha mada za majopo matano yatakayojadili na kuzungumzia, (i). Upatikanaji na kuweza kumudu mbadala wa Biomasi (kuni na mikaa), (ii). Je, tunaweza kupeleka gesi ya kupikia nyumbani (LPG) kwa wananchi? (iii). Nishati ya Kupikia na Ustawi wa Wanawake, (iv). Ugharimiaji wa Nishati Safi ya Kupikia (v). Mtazamo wa afya kwenye matumizi ya nishati ya kupikia.

Ujerumani yaungana na Mataifa ya Afrika UN
Waziri Mchengerwa ataka ushindi Kimataifa