Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema kuwa Serikali yake ya awamu ya sita imetoa kipaumbele katika kuendeleza miradi ya maendeleo ya serikali ya awamu ya tano na kukiri kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Akizungumza katika mahojiano maalum na kituo cha Televisheni cha Taifa TBC Rais Samia ameelezea miradi ya maendeleo inavyoendelea ikiwemo mradi wa Reli ya umeme SGR ambapo ametia saini kwa Swaum ya 5 ya kuendeleza mradi na aliweka jiwe la msingi kuashiria kazi inaendelea.
“Nilichukua nafasi au dhamana tukiwa na Roti mbili ya Dar es Salaam-Morogoro, Mororgoro -Makutupora- Singida na kukawa kumeshamalizwa mambo yote ya “Roti five” ikabakia kusaini na kukubaliana kuendelea na kazi, nilianza kusaini Roti five tukaendelea na kazi tukaweka jiwe la msingi tukaendelea na kazi,” Amesema Rais Samia.
“Baadae tena tukatangaza tenda ya sehemu ya tatu na ya nne kutoka Makutupora kwenda Tabora, Tabora kwenda Mwanza ambayo tayari Makutupora , Tabobara tumeshapata mkandarasi yuko site, kutoka Tabora kwenda Mwanza tayari tulishatangaza shuhuli za manunuzi zinaendelea kumpata mkandarasi ili aendelee,” Ameongeza Rais Samia.
Rais Samia amesema kuwa sehemu ya sita ya mradi inatarajiwa kutangazwa ili kupata mkandarasi atakaejenga kutoka Tabora mpaka Kigoma, huku akisema nia ya ujenzi wa reli hiyo ni kuunganisha nchi za Afrika Mashariki.
“Nia ya Reli tufike Kigoma mpaka Burundi kuunganisha na Rwanda ili DRC Congo wachukue Burundi waendelee kwao ili tupate soko la DRC kwa urahisi,” Amesema Rais Samia.
Akizungumzia mradi mwingine wa urithi kutoka serikali ya awamu ya tano ambayo ni Ujenzi wa bwawa la Mwalimu Nyerere, Rais Samia amesema kuwa mradi unaendelea vizuri ambapo kwa sasa umefikia asilimia 60 ya maendeleo kutoka asilimia 46 ya ujenzi licha ya kukiri kusimama kwa mradi huo kutokana na sababu mbalimbali ikwemo janga la uviko 19 na kupelekea mradi huo kukamili mwaka 2024 badala ya mwaka 2022.
Sambamba na hayo pia amegusia mradi wa Daraja la Busisis ambao pia amekiri kuendelea vizuri na sasa upo kati ya asilimia 36 kukamilika kutoka asilimia 20 za mradi tangu kuupokea kutoka serikali ya awamu ya tano, lakini ujenzi wa barabara sehemu mbalimbali nchini unaendelea ikiwa ni juhudi za kuendelea kukamilisha miradi ya maendeleo na kuendelea kuleta miradi mingine ya maendeleo.