Kinshasa, DRC Rais wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Felix Tshisekedi Tshilombo, hapo jana Jumapili Aprili 14, aliwasili jijini Goma, mkoa wa Kivu Kaskazini ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kwanza ndani ya nchi hiyo tangu kuchaguliwa kwake mnamo mwezi Desemba mwaka jana.
Rais Tshisekedi anazuru jimbo la Kivu, eneo ambalo limeendelea kukumbwa na ukosefu wa usalama na maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.
Ziara hiyo ilianzia mjini Lubumbashi ambako Rais Tshisekedi alikutana na viongozi wa sekta mbalimbali katika mkoa huo.
Aidha, watu wengi wamekuwa wakijiuliza maswali bila kupata majibu ya kuwa kwanini baada ya kuapishwa kwake kipaumbele cha rais Tshisekedi kimekuwa ni ziara za nje kuliko za ndani?.
Tangu kuapishwa kwake Januari mwaka huu Tshisekedi ameshafanya ziara kadhaa katika mataifa zaidi ya 5, ikiwa ni pamoja na nchi jirani ya Rwanda na Uganda bila kusahau Kenya ambapo Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta alihudhuria sherehe ya kuapishwa kwake mjini Kinshasa.
Hata hivyo, tangu kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa DRC, Tshisekedi hajatangaza baraza lake la mawaziri, ijapo kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na ikulu ya Kinshasa serikali mpya inatarajiwa kutangazwa hivi karibuni.