Rais wa Jamhuri ya Malawi  Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera anatarajia kufika nchini kesho kwa ajili ya kufanya ziara ya kitaifa ya  siku tatu, kuanzia Oktoba  7 mpaka 9 2020,  yenye lengo la kuimarisha uhusiano,  ushirikiano  na kuendelea kudumisha ujirani uliopo baina ya nchi hizi mbili

Dkt. Chakwera atapokelewa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli katika uwanja wa ndege wa Julius Kambarage Nyerere jijini Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Chakwera atatembelea bandari ya Dar es Salaam ili kujionea shughuli mbalimbali na uboreshaji wa miundombinu ya bandari hiyo na  kituo cha kuhifadhia mizigo cha Malawi (Malawi Cargo Center) ambacho kimekuwa alama muhimu ya ushirikiano kati ya Tanzania na Malawi.

Aidha, Dkt. Chakwera akiwa na mwenyeji wake rais Magufuli  wataweka jiwe la msingi katika kituo cha mabasi yaendayo mikoani cha Mbezi kama ishara ya ushirikiano na umoja katika uendelezaji wa miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi amesema uhusiano kati ya Tanzania na Malawi ni wa muda mrefu na unaendelea kuimarika siku hadi siku ambapo nchi hizi mbili zimeendelea kushirikiana katika nyanja za kisisasa, ulinzi na usalama, kiuchumi,  kijamii na masuala ya kikanda.

Kwa upande wake  mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Abubakar Kunenge  amewataka wakazi wa jiji la Dar es Salaam wawe tayari kwa ajili ya ugeni huo na wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kumpokea  rais Chakwera.

Hii inakuwa ni ziara rasmi ya kitaifa  ya kwanza kwa rais Chakwera tangu aingie madarakani mwezi Juni mwaka huu  ambapo kabla amefanya ziara za kikazi za siku moja moja katika nchi za Zambia na Zimbabwe.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Oktoba 7, 2020
Zitto kabwe apata ajali