Kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria chini ya umri wa miaka 16, kilichotwaa ubingwa wa fainali za kombe la dunia za mwaka 1985, kimezawadiwa bahshishi kama asante, ikiwa ni baada ya miaka 30.

Kikosi hicho kimetunzwa fedha na rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari ambaye aliahidi kufanya hivyo alipokuwa kiongozi wa kijeshi wakati wa michuano hiyo ya 1985.

Nduka Ugbade, nahodha wa timu hiyo iliyolaza Ujerumani Magharibi kwenye mchezo wa hatua ya fainali mjini Beijing, amethibitisha kupokea sehemu ya fedha za zawadi, alipozungumza na shirika la utangazi la Uingereza BBC.

Amesema amefurahi sana, kutokana na rais wake kutimiza ahadi aliyoitoa miaka kadhaa iliyopita.

Buhari alikuwa amewaahidi wachezaji hao nyumba, hisa katika benki kuu na ufadhili wa kimasomo ikiwa ni miongoni mwa zawadi nyingine, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na serikali yake kupinduliwa.

Buhari, aliyechaguliwa kuwa rais mwaka jana, alitangaza Januari mwaka huu kwamba atatoa zawadi ya naira milioni mbili ambazo ni sawa na dola za kimarekani 10,000, au Paund za kiingereza 7,000  kwa kila mchezaji na naira million 1.5 kwa maafisa wa timu.

Baada ya wachezaji kupewa pesa zao, walikaa kimya dakika moja kukumbuka kifo cha mwenzao Kingsley Aikhionbare ambaye ameshaaga dunia tangu mwaka 1996 akiwa jijini London nchini England.

Mashindano yao ya ubingwa wa dunia wa wachezaji wa chini ya miaka 16 yaliandaliwa mara tatu kabla ya kubadilishwa na kuwa Kombe la Dunia kwa wachezaji wa chini ya miaka 17 mwaka 1991.

Nigeria walishinda Kombe la Dunia la wachezaji wa umri wa chini ya miaka 17 mnamo 1993, 2007, 2013 na 2015.

Sunday Oliseh Aachia Ngazi Nigeria
FIFA Kumpata Rais Mpya Hii Leo