Tume ya uchaguzi Zanzibar (ZEC), imemteua Maalim Seif Shariff Hamad kuwa mgombea wa urais wa Zanzibar kupitia chama cha ACT Wazalendo katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu baada ya kuona mapingamizi aliyowekewa Seif hayana mashiko.
Mapingamizi hayo yaliwekwa na vyama vya DP na Demokrasia makini wakidai fomu za Maalim Seif zina kasoro.
Akitoa taarifa hiyo Mwenyekiti wa ZEC, Hamid Mahamoud Hamid, amesema Maalim sasa anaruhusiwa kuendesha kampeni kwa mujibu wa sheria, kanuni, miongozo ya tume na ratiba ya kampeni.
Maalim seif alikuwa miongoni mwa wagombea 17, waliokuwa wamechukua fomu kuwania urais Zanzibar lakini Septemba 10, 2020 ulifanyika uteuzi wa wagombea 16, Maalim Seif akiwekewa pingamizi. Kampeni za Uchaguzi mkuu Zanzibar, zinatarajiwa kuzinduliwa leo Septemba 12, 2020.