Uongozi wa klabu ya Everton, umeonyesha msimamo wa kutokukubali kirahisi kumuuza mshambuliaji wao kutoka nchini Ubelgiji, Romelu Menama Lukaku kuelekea dirisha la usajili ambalo litakua wazi mara baada ya msimu wa 2015-16 kufikia kikomo mwezi ujao.

Uongozi wa klabu hiyo ya Goodson Park, umetangaza msimamo huo kutokana na ofa zilizoelekezwa kwa Lukaku ambaye msimu huu ameonesha kuwa katika kiwango cha hali ya juu cha kuzifumania nyavu za timu pinzani.

Klabu za Manchester United, Chelsea, Paris Saint-Germain, Real Madrid pamoja na Bayern Munich zimetajwa kuwa katika harakati za kuiwani saini ya mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 22.

Ofa kubwa ambayo inakadiriwa kufikia kiasi cha Pauni million 65, imetiliwa mashaka na viongozi wa Everton kwa kuonekana haina thamani ya Lukaku kwa sasa, hivyo imeshauriwa wenye mpunga huo kuuongeza zaidi.

Hata hivyo haijatajwa ni klabu gani imefikia kuweka kiasi hicho cha pesa, ambacho iliamini kingewashawishi viongozi wa Everton kukubali kirahisi kumuachia Lukaku mwishoni mwa msimu huu.

Msimamo uliopo huko Goodson Park kwa sasa, ni kuona Lukaku anasajiliwa kwa ada itakayokaribia rekodi ya usajili iliyowekwa na Gareth Bale mwaka 2013 alipokua akisajiliwa na klabu ya Real Madrid akitokea Tottenham Hotspurs.

Kama mpango huo utaonekana kushindwa kufua dafu, viongozi hao wameibuka na njia ya pili kama mbadala ya kutaka kuona mchezaji wao anakua katika tano bora ya wachezaji waliosajiliwa kwa kiasi kikubwa cha pesa duniani.

Kwa sasa orodha hiyo inaongozwa na Gareth Bale, akifuatiwa na Cristiano Ronaldo, Neymar pamoja na Luis Suarez ambao wote wanacheza katika ligi ya nchini Hispania.

Rekodi ya usajili iliyoweka duniani mwaka 2013, ilifikia kiasi cha Pauni million 85.3 baada ya Real Madrid kumsajili Gareth Bale.

Nape Aahidi Kusimamia Nyasi Bandia Za Uwanja Wa Nyamagana
Salum Bausi Aipa Mtihani Mzito Kamati Ya Uchaguzi ZFA