Serikali ya Lebanon, imewafungulia mashtaka watu saba kwa kuhusika na shambulizi dhidi ya askari wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, lililomuua mwanajeshi mmoja wa Ireland katikati ya mwezi Desemba, 2022.
Katika tukio hilo, askari Sean Rooney (23), aliuawa na wenzake watatu kujeruhiwa wakati gari la Jeshi la muda la Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL), liliposhambuliwa karibu na kijiji cha Al-Aqbiya, ambayo ni ngome kuu ya kundi la washia la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran.
Jeshi la Muda, la Umoja wa Mataifa nchini Lebanon liliitaka Serikali jijini Beirut kuhakikisha uchunguzi unafanyika haraka, kuhusu kifo cha kwanza cha mmoja wa walinda amani wake kwa karibu miaka minane.
Mohammad Ayyad ndiye aliye kizuizini pekee kati ya watu saba walioshitakiwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo la Desemba 14, 2022 na Hezbollah ndiyo ilimkabidhi mtu huyo kwa jeshi la Lebanon mwezi uliopita (Desemba, 2022).