Aliyekua kiungo wa Man Utd, Paul Scholes, ameuponda mfumo wa meneja wa klabu hiyo Louis van Gaal, kwa kusema katu asingeweza kucheza chini ya utawala wake.

Scholes, ambaye kwa sasa anafanya shughuli ya uchambuzi wa soka kupitia kituo cha televisheni cha Bt Sports, amefikia hatua ya kulizungumza jambo hilo, kutokana na kuchoshwa na mwenendo wa kikosi cha Man Utd unaonekana kwa sasa.

Hatua ya kufungwa na Middlesbrough katika mchezo wa kuwania kombe la ligi uliochezwa siku ya jumatano, ndiyo imekua chanzo cha gwiji huyo kuyatoa ya moyoni kwa kuuponda mfumo wa Van Gaal, ambaye alionekana kuwa mkombozi wa Man utd.

Amesema mfumo wa meneja huyo kutoka nchini Uholanzi umeonyesha kufeli kwa kiasi kikubwa, katika michezo miwili mfululizo iliyochezwa siku za karibuni, hasa pale ilipoonekana akiwatumia washambuliaji wawili Wayne Rooney pamoja na Anthony Martial.

Scholes ameongeza kwamba, jambo la ubunifu pia limekua kikwazo kwenye kikosi cha Man Utd, hali ambayo inapelekea baadhi ya mambo kutosogea huko Old Trafford.

Scholes, alikua sehemu ya kikosi cha Man Utd kilichopata mafanikio ya kutwaa ubingwa wa ligi ya England mara 11, ligi ya mabingwa barani Ulaya mara mbili, ubingwa wa kombe la FA pamoja na ubingwa wa kombe la ligi mara mbili.

Kevin MacDonald Arejesha Vijembe Kwa Mahasimu
Gus Poyet Alamba Ajira Ugiriki