Wizara ya Maliasili na Utalii kupitia Idara ya Mambo ya Kale imeanza mkakati maalum wa kuainisha, kuhifadhi na kuyatangaza maeneo ya kihistoria yanayopatikana Mkoani Dodoma, ikilenga kulifanya Jiji hilo kuwa na vivutio vya kitalii sawa na maeneo mengine Duniani.
Hatua hiyo inafuatia kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mohammed Mchengerwa kuwa Tanzania imebariki kuwa na vivutio vya utalii vya kila aina mbali na wanyamapori na endapo watumishi atawajibika ipasavyo idadi ya watalii itaongezeka maradufu, ifikapo mwaka 2025.
Mkurugenzi wa Idara ya Mambo Kale, Dkt. Christowaja Ntandu alihamasika kutembelea mnara wa Uhuru, Mnara wa Mashujaa wa Tanzania, Nyerere square na Hoteli ya Dodoma, na kusema lengo ni kuongeza mazao mapya ya Utalii hasa ya utalii wa Malikake kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Maeneo mengine aliyotembelea ni pamoja na eneo Kikuyu ambalo lina asili ya jina la Dodoma, Mti aina ya Mkuyu uliopo katika eneo la Chuo Kikuu cha St. John ambao ulitumika kunyongea wahalifu wakati wa Utawala wa Wajerumani na Makaburi ya Wahanga wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia.