Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema kuwa Serikali haitakubaliana na mtumishi yeyote wa umma atakayefanya urasimu kwa lengo la kukwamisha uboreshaji wa sekta binafsi kwani inahitaji ushirikiano mkubwa na wafanyabiashara.

Amesema miongoni mwa maboresho yanayofanywa na Serikali katika sekta binafsi ni pamoja na kuimarisha utendaji wa watumishi na kuondoa urasimu katika utendajikazi wa kila siku baada ya eneo hilo limelalamikiwa sana.

Majaliwa amesema hayo Desemba 2, 2016 wakati akizungumza na wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda mkoani Arusha kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Arusha (AICC) akiwa katika siku ya kwanza ya ziara ya kikazi mkoani Arusha.

“Serikali inafanya jitihada kubwa katika kuhakikisha inaweka mazingira mazuri ya uwekezaji ili kukuza uchumi wa nchi yetu. Pia mapambano dhidi ya rushwa yanayofanyika ndani ya Serikali na nje yanalenga kuleta maboresho makubwa katika sekta binafsi ,” alisema.

Alisema Serikali inawataka watendaji wake wote watumie lugha nzuri na rafiki katika kutoa huduma kwa wafanyabiashara na wananchi kwa jumla na haitamvumilia mtumishi yeyote atakayefanya urasimu ili mfanyabiashara atoe rushwa.

“Hatuwezi kuzungumzia maendeleo katika sekta za maji, madini na viwanda bila ya kutaja wafanyabiashara kwa sababu hata viwanda wao ndiyo wamiliki. Wafanyabiashara wameondoa vijana wengi waliokuwa wanakaa vijiweni na kujadili mambo yasiyokuwa na tija na kuwaajiri kwenye viwanda vyao,” -Majaliwa

Riphat Hamisi Mchezaji Bora Wa VPL Mwezi Novemba, 2016
Ni nani msanii wa hip hop namba 1 Tanzania? Nikki wa Pili afunguka