Serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeikabidhi halmashauri ya wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe msaada wa pikipiki 21 zenye thamani ya milioni 63 kwa ajili ya maafisa elimu ngazi ya kata ili kurahisisha utekelezaji wa shughuri za elimu sambamba na kukuza kiwango cha elimu.
Akizungumza katika zoezi la makabidhiano ya pikipiki hizo kutoka TAMISEMI Salumu Mkuya,amesema serikali inatambua changamoto ya usafiri iliyokuwa ikiwakabili maafisa elimu nchini na kuamua kutoa pikipiki kwa ajili ya kufika kila kata kwa wakati ili kuinua kiwango cha elimu.
“Hizi pikipiki mmepewa mfike kila kata hata zilizopo pembezoni muende mkainue kiwango cha elimu….mlete mabadiliko cha chanya ya kuinua ufaulu” amesema Mkuya.
Aidha, ametoa rai kwa maafisa hao kuhakikisha wanavitunza na kwamba serikali inatendelea kuboresha sekta ya elimu ili kuzalisha wataalamu watakaotumiwa kwenye uchumi wa viwanda.
Naye mkuu wa wilaya ya wanging’ombe Ally Kassinge,amewataka maafisa hao kutumia pikipiki hizo kuchochea kupanda kwa ufaulu na zisitumike tofauti na dhamira ya serikali kuu.
“Pikipiki hizi lengo lake ni kwenda kuchochea ufaulu na si kwamba mkazitumie tofauti na dhamira ya serikali…mvitunze kikipotea kimepotea chako inamaana ikitokea tu utawajibika” amesema Kassinge.
Jumla ya pikipiki 106 zimetolewa kwa Mkoa wa Njombe zenye thamani ya milioni 318 ambapo Makete 23, Ludewa 25, Makambako 12, Njombe wilaya 12, Njombe Mji 13.