Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema inaendelea kuongeza nguvu katika kutangaza utalii na vivutio vyake vilivyopo nchini Tanzania kama njia mojawapo ya uimarishaji wa sekta hiyo.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana alipokuwa akiongea mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii.
Amesema, hayo yanafanyika kupitia maonesho na mikutano mikubwa ya Kimataifa, kama ule wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani kamisheni ya Afrika (UNWTO-CAF) uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha na Onesho la Kimataifa la Utalii la Swahili ‘Swahili International Tourism Expo’ (SITE) lililofanyika jijini Dar es salaam.
Aidha, Waziri Chana pia ameipongeza Kamati hiyo kwa kazi kubwa ya kuisimamia Serikali kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, huku akiishukuru Kamati hiyo kwa ushirikiano inaoutoa kwa Wizara.
Hata hivyo, ameihakikishia Kamati kuwa Wizara itaendelea kuufanyia kazi ushauri unaotolewa na Kamati hiyo, ili kuendeleza sekta ya Maliasili na Utalii kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.