Serikali imepiga marufuku wanafunzi wanaoanza elimu ya msingi (darasa la kwanza) kudaiwa vyeti vya elimu ya awali, kwa maelezo kuwa hakuna sera inayoelekeza shule za awali kutoa vyeti hivyo.
Marufuku hiyo imetolewa na Waziri wa TAMISEMI, Ummy Mwalimu bungeni jijini Dodoma leo wakati akitoa jibu la nyongeza kufuatia swali lililoulizwa na Mbunge Mariamu Kisangi ambaye alitaka kujua kutokana utaratibu wa vyeti hivyo kutakiwa, serikali ina mpango gani kuhakikisha elimu hiyo inatolewa kwa wanafunzi wote.
“Ni marufuku shule kudai certificates (vyeti) za awali kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza, bado hatujafanya vizuri katika kuongeza access (upatikanaji) ya watoto kuanza elimu ya awali. Kwa hiyo haileti mantiki kusema kila mtoto aanze darasa la kwanza awe na certificate ya awali,” amesema Waziri Ummy.
Hata hivyo ameahidi kuwa serikali itaweka nguvu kuhakikisha kuwa watoto wanapata elimu ya awali hususani katika maeneo ya vijijini.
“Wote ambao wanadai certificate ya elimu ya awali wajue kwamba wanatenda kinyume na maelekezo na miongozo ya serikali,” amesema Waziri Ummy.