Wakala wa Jiolojia Nchini (GST) imezitaka Taasisi za Umma, Wizara na Idara za Serikali kuwatumia Wataalamu wa jiolojia katika shughuli za ujenzi wa ofisi za Serikali Mkoani Dodoma ili
kuweza kukabiliana na athari za matetemeko ya ardhi yanayotokea mara kwa mara Mkoani humo.
Wito huo umetolewa  na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Nchini(GST) Profesa Abdulkarim Mruma,  kuhusiana na athari zitokanakazo na mabadiliko ya tabia nchi  ikiwemo matetemeko ya ardhi hususani katika kipindi hiki ambacho Serikali imepanga kuhamishia shughuli zake mkoani Dodoma.
“Nashauri Serikali kutuma wataalamu kufanya utafiti ili kuangalia ni maeneo gani yanafaa kujenga ofisi za Serikali na zinatakiwa zijengwe kwa mfumo upi ili ziweze kuhimili matetemeko ya ardhi pindi yanapotokea” alisema Profesa Mruma
Aliongeza kuwa hapo awali ujenzi wa magorofa mkoani humo ilikuwa mwisho  ghorofa nne kutokana na mkoa huo kupitiwa na Bonde la Ufa la Afrika Mashariki ambalo kusababisha matetemeko ya mara kwa mara.
“Jengo likiwa jembamba na refu ni rahisi kupata madhara pindi tetemeko linapotekea hivyo ni vyema watu wafuate ushauri wa wataalamu kabla kufanya ujenzi na pia kuangalia maeneo yanayofaa kwa ujenzi” alisema Prof Mruma
Aidha ameongeza kuwa majengo yote yatakayojengwa yanatakiwa kuzingatia ubora wa majengo kwa kutumia wataalamu badala ya kujenga bila kushirikisha wataalamu.

Video: Mrema awageukia wanaopinga Serikali kuhamia Dodoma
Waziri Mkuu azindua miongozo ya Mfumo wa Anwani za Makazi