Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Omar Mgumba ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), kufanya uchunguzi wa matumizi ya fedha kwenye mradi wa ujenzi wa hospitali ya Wilaya ya Mkinga, kutokana na kuhisi uwepo wa ubadhirifu wa fedha.
Kauli hiyo, ameitoa wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo, ambayo inatekelezwa katika Wilaya ya Mkinga, baada ya kutoridhishwa na taarifa iliyotolewa ya utekekezaji wa mradi huo, sambamba na kutokuwepo kwa nyaraka muhimu wakati wa ukaguzi wa mradi huo.
Amesema, kukosekana kwa nyaraka za muongozo wa matumizi ya fedha kwenye mradi huo, sambamba na mwongozo wa utaratibu wa Ujenzi wa mradi (BOQ), inaonesha wazi kuna harufu ya matumizi mabaya ya fedha.
Mgumba ameongeza kuwa, “Nilishatoa maelekezo kuwa nikija kwenye ukaguzi wa miradi katika wilaya husika, nitafanya kama vile miradi ya Mwenge inavyokaguliwa, nataka nikute nyaraka zote kwenye eneo la mradi na sio kuambiwa zipo ofisini.”
Awali, msimamizi wa mradi huo, Stewart Matai, alisema mradi huo ulitakiwa ukamilike Agosti mwaka huu, lakini changamoto ya ukosefu wa maji,iliwalazimisha kusimamisha ujenzi.