Hatimaye Serikali imetoa jibu lililokuwa likisubiriwa na watu wengi kuhusu mshahara aliokuwa analipwa Rais wa Serikali ya Awamu ya Nne, Dk. Jakaya Kikwete.

Awali, taarifa mbalimbali zilizotolewa na watu pamoja na viongozi wa vyama vya upinzani zilidai kuwa Dk. Kikwete alikuwa analipwa shilingi milioni 34 kama mshahara kila mwezi, taarifa ambazo zilikuwa zikikanushwa na Ikulu bila kutaja kiwango sahihi.

Serikali kupitia Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora imeweka wazi mshahara aliokuwa anaupokea Dk. Kikwete ikiwa ni siku chache baada ya Rais John Magufuli kupiga simu katika kituo cha runinga cha Clouds TV na kuweka wazi mshahara wake huku akisisitiza kutoa nyaraka zake punde atakaporejea kutoka mapumzikoni nyumbani kwake Chato.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, Dk Laurian Ndumbaro, amesema kuwa Wizara hiyo ndiyo yenye dhama ya mishahara ya watumishi wote wa umma ikiwa ni pamoja na viongozi, na kwamba mishahara huidhinishwa kupitia bajeti za mwaka zinazopitishwa na Bunge kila mwezi Juni.

Hivyo, kwakuwa Rais Magufuli aliingia maradakani kabla ya kumalizika kwa Mwaka wa Fedha 2015/16, aliendelea kulipwa mshahara uleule aliokuwa analipwa Dk. Kikwete katika nafasi hiyo ya kiti cha Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Kwa hiyo, bajeti hiyo iliidhinishwa kwa viongozi wote, Rais, Makamu wa Rais, wabunge na watumishi wote wa umma. Hivyo, mshahara wa Rais, kwa mantiki hiyo, Rais Kikwete (Jakaya) ndio huo ambao unatumiwa na Rais John Magufuli. Kama mshahara, hakuna tofauti, hakuna mabadiliko, kiwango ni kile kile. Rais mpya hakutengenezewa mshahara mpya,” alifafanua Katibu Mkuu huyo wa Utumishi na Utawala Bora.
Rais Magufuli alisema kuwa anapokea mshahara wa shilingi milioni tisa na laki tano kwa mwezi (9,500,000). Kutokana na maelezo ya Katibu Mkuu huyo, Dk. Kikwete pia alikuwa anapokea kiasi hicho cha fedha.

Rais Zuma anusurika Bungeni
Kaimu Mkurugenzi Wa Mashindano Wa TFF Ajiuzulu