Serikali kupitia Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), Bodi ya Filamu na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA) imefanikiwa kuzindua mifumo ya kidijitali ya Usajili na utoaji wa vibali kwa wasanii na wadau wengine wa sanaa unaojulikana kama Artist Management Information System (AMIS) ambao unarahisisha kukamilisha hatua zote za kujisajili, kulipia vibali na kupokea vyeti vya kutambuliwa wakiwa popote walipo nchini au nje ya nchi.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mohamed Mchengerwa leo Machi 16, 2022 wakati akiwasilisha taarifa ya Mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, huku akieleza lengo la mfumo huo kuwa ni kuboresha na kurahisisha ufanyaji kazi wa wadau wa sekta hiyo.

“Kupitia Taasisi ya Haki Miliki Tanzania (COSOTA), ikiwa ni baada ya takribani miaka minne, imelifanyia kazi suala la mirabaha ya wasanii na kuongeza mapato ya mirahaba kutokana na makusanyo ya maonesho kwa umma na utangazaji yaliyofanyika kati ya zaJulai 1 hadi Disemba 31, 2021, ambapo jumla ya Shilingi milioni 312.29 zilikusanywa na kugawanywa. Hiki ni kiasi kikubwa kuwahi kugawiwa ambapo kazi za Sanaa 5,924 zilizofuzu vigezo vya kupata mirabaha ambapo jumla ya wasanii 1,123 walinufaika” Amesema Waziri Mchengerwa.

Aidha Waziri Mchengerwa amsema Wizara kwa kushirikiana na Kituo cha Sanaa na Utamaduni kwa Viziwi Tanzania (KISUVITA) imefanikiwa kuratibu na kukamilisha mashindano ya urembo na mitindo kwa Viziwi yaliyofanyika mwezi Agosti 2021, ambapo Watanzania sita kati ya washiriki 74 kutoka zaidi ya nchi 15 za Afrika walifikia vigezo vya kushiriki mashindano ya dunia yaliyokuwa yamepangwa kufanyika nchini Brazil, hata hivyo baada ya Tanzania kuonesha ufanisi katika mashindano hayo ngazi ya Bara la Afrika, imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa Mashindano hayo ya dunia yenye washiriki zaidi ya 300 yanatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba 2022 .

Siri ya Hayati Magufuli na Mafisadi yafichuliwa
Mwanahabari mwingine auwawa Ukraine