Klabu ya Simba SC kesho Jumatano (Julai 27) itacheza mchezo mwingine wa Kimataifa wa Kirafiki ikiwa ni muendelezo wa maandalizi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika.

Simba SC imethibitisha taarifa za kutarajiwa kucheza mchezo huo wa Kirafiki kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii, ambapo imekua njia sahihi ya kuwafikishia ujumbe Mashabiki na Wanachama wake.

Taarifa iliyoandikwa kwenye kurasa za mitandao ya kijamii ya Simba SC imeeleza kuwa kesho Jumatano kikosi cha Msimbazi kitacheza dhidi ya Haras El Hodoud.

Mchezo huo umepangwa kucheza mjini Cairo, ambapo kikosi cha Simba SC kitalazimika kusafiri kutoka mjini Ismailia kilipoweka kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa 2022/23.

“Kesho Jumatano tutakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya klabu ya Haras El Hodoud ambao utapigwa jijini Cairo” imeeleza taarifa ya Simba SC

Simba SC imeshacheza michezo miwili ya Kirafiki tangu ilipoanza kambi nchini Misri majuma mawili yaliyopita, mchezo wa kwanza walikipiga Ismailia FC wakaambulia sare ya 1-1 kisha wakacheza dhidi ya Abou Hamad waliokubali kufungwa 6-0.

Serikali yataifisha dawa za binadamu aina 34
Rais Samia alia ajali Mtwara