Uongozi wa Klabu ya Simba SC umeweka wazi kuwa mchezo wao wa Mzunguuko wasita wa Kundi C, Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Raja Casablanca ni wakusaka heshima kwa kuwa malengo ya kutinga Robo Fainali yameshatimia.

Simba SC chini ya Kocha Mkuu, Roberto Oliveira ina kibarua cha kukamilisha kete ya mwisho dhidi ya Raja mchezo unaotarajiwa kuchezwa Aprili Mosi mjini Casablanca nchini Morocco.

Kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa Simba SC ilikubali kichapo cha 0-3, ukiwa ni mchezo ambao waliruhusu mabao mengi kwenye hatua ya makundi msimu huu 2022/23.

Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba Ahmed Ally, amesema kuwa mchezo wao wa mwisho una umuhimu licha ya malengo kukamilika.

“Tulikuwa na hesabu ndefu kwenye kila mchezo hasa Horoya AC na Vipers hawa ilikuwa ni lazima wafufue matumaini yetu kutinga hatua ya Robo Fainali na mwisho kila kitu kimekamilika.”

“Kazi yetu dhidi ya Raja Casablanca sio nyepesi kwani walipokuja nyumbani walitufunga kwenye mchezo ambao tulikuwa tunahitaji ushindi na sasa tunawafuata wao kusaka heshima kwa ajili ya wachezaji na mashabiki kwani ni mchezo wetu wa mwisho.”

“Raja tunawaheshimu ni timu bora na imeshatinga hatua ya robo fainali tutachukua tahadhari zote kwenye mchezo huo mashabiki wazidi kuwa pamoja nasi,” amesema Ally

Simba SC imeshavuka Hatua ya Makundi na kutinga Hatua ya Robo Fainali ikiwa na alama 09, ikitanguliwa na Raja Casablanca inayoongoza Kundi C kwa kuwa na alama 13, huku Horoya AC ya Guinea ikifikisha alama 04 na Vipers SC ya Uganda ikiendelea kuburuza mkia kwa kuwa na alama 02.

Shujaa filamu ya Hotel Rwanda kuachiliwa huru
Ligi ya Championship kurushwa Live