Saa chache baada ya Mabingwa wa Soka Barani Afrika Al Ahly kumtambulisha kiungo mshambuliaji kutoka nchini Msumbiji Jose Luis Miquissone, Uongozi wa Simba SC umemtakia kila la kheri mchezaji huyo.

Simba SC imemtakia kheri zote Miquissone kwa kuandika waraka maalum na kuusambaza kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Waraka wa Simba SC umeandikwa: Uongozi wa Simba umemtakia heri na mafanikio mchezaji Luis Miquissone baada ya kujiunga na klabu Al Ahly ya Misri. Simba inashukuru kwa mchango wake ndani ya kikosi chetu na akiwa nasi amefanikiwa kutwaa mataji mawili ya Ligi Kuu, mataji mawili ya FA, na Ngao ya Jamii mara moja na tuzo binafsi kama mchezaji bora wa mwezi mara kadhaa.

Simba inaamini Luis ataendelea kufanya vizuri akiwa na timu yake mpya kutokana na uwezo mkubwa alio nao pamoja na nidhamu ya ndani na nje ya uwanja.

Tunaamini Luis ataendelea kuwa mwanafamilia na Balozi wa Simba siku zote.

Imetolewa na Idara ya Habari na Mawasiliano
Simba Sports Club
Agosti 26, 2021

Taarifa za Manara zatikisa Misri
Billioni 118 kunusuru kaya masikini mradi wa TASAF