Mechi ya mpira wa kandanda ya klabu za nyumbani itaonyeshwa moja kwa moja kupitia runinga kwa mara ya kwanza katika historia ya Somalia leo.

Fainali ya kombe la Jenerali Da’ud kati ya timu ya Jeshi la Somalia Horseed na ile ya idara ya Polisi Heegan itaonyeshwa moja kwa moja na runinga ya taifa ya Somalia.

Rais wa shirikisho la mchezo wa soka nchini Somalia, Abdiqani Said Arab, ametaja hatua hiyo kama historia kwa taifa hilo na afueni kwa ukuaji wa mchezo huo nchini humo.

Somalia ingali inajaribu kujinasua kufuatia vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miongo miwili.

”Tulikuwa na ndoto kuwa siku moja mechi zetu zitaonyeshwa moja kwa moja kwenye runinga, na huu ni mwanzo wa ndoto hiyo kutimia’,” anasema Said Arab.

Anaongeza kusema kuwa mechi hiyo ni jaribio lao la kwanza na ikiwa litafanikiwa, watajaribu kuonyesha mechi nyingine miezi ijayo.

Michuano ya kuwania kombe la Jenerali Da’ud ndiyo ya pili katika michezo kwa kuvutia mashabiki wengi nchini humo.

Shindano hilo hufanyika kila mwaka na limepewa jina hilo kutokana na mwanzilishi wa Jeshi la Somalia, Jenerali Da’ud Abdulle Hersi.

Jenerali Da’ud, alifariki mwaka wa 1965 na serikali ya Somalia imekuwa ikiandaa na kufadhili kombe hilo la soka tangu mwaka wa 1972.

Niyonzima Afungiwa Kucheza Soka La Bongo
TFF Yafungua Milango Kwa Wenye Vibali Vya Kimataifa