Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye amekosoa mwenendo wa Serikali ya Awamu ya Tano akipinga baadhi ya hatua zinazochukuliwa kupitia tasnia ya habari.

Akiongea jijini Dar es Salaam wakati dunia ikiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, Sumaye amesema kuwa anashangaa kuona viongozi wa serikali wakiwa hawapendi kukosolewa na badala yake wanapenda kusikia wakisifiwa pekee. Sumaye alisema kuwa hizo ni sifa za udikteta.

Amesema kuwa serikali inakosea kuminya uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa watu kutoa maoni yao na kwamba kufanya hivyo kunaashiria kuwa inaficha ‘madudu’.

“Wapo Watawala ambao hawapendi kusemwa lakini wanapenda sana kusifiwa. Kiongozi mwenye tabia ya udikteta hataki kusikia kingine zaidi ya sifa zake tu. Huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,” anakaririwa.

Aidha, alikosoa hatua ya Serikali kuzuia kurushwa moja kwa moja kwa vikao vya Bunge kupitia vyombo vya habari akisema kufanya hivyo ni kuvunja Katiba ya nchi.

“Unapoondoa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge, kwanza ni kuvunja katiba. Ibara ya 18 (d) ya Katiba inasema, kila mtu ana haki ya kupewa taarifa wakati wote. Kwa kuzuia Bunge kuoneshwa ‘live’ wewe serikali unataka kutoa taarifa ya Bunge kwa wakati unaoutaka na kwa taarifa unayoitaka wewe,” alisema.

Aliongeza kuwa hoja ya serikali kutorusha live vikao vya Bunge ili kubana matumizi ni dhaifu kwani kutofanya hivyo kumeongeza gharama kwakuwa imewalazimu kununua vifaa vya studio na kuajiri wafanyakazi wake watakaoshughulikia kurushwa kwa Bunge.

 

Waziri Mahiga atoa ya moyoni kuhusu sakata la mkewe na trafiki
Rufaa Ya Geita Gold Sports Yagonga Mwamba TFF