Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk. Augustine Mahiga amevunja ukimya na kuzungumzia sakata maarufu la ‘vutankuvute’ kati ya mkewe na askari wa usalama barabarani lililopelekea Rais John Magufuli kuamuru askari huyo apandishwe cheo.

Dk. Mahiga amemtetea mkewe na kueleza kuwa hakumtukana hata kidogo askari huyo na kwamba kilichotokea ni kupishana kauli wakati wa mazungumzo na sio vinginevyo.

Balozi Mahiga alieleza kuwa amefuatilia kwa karibu na kusikiliza kipande cha sauti kinachosambaa kwenye mitandao ya kijamii, chenye mazungumzo kati yao na hakuna tusi alilolisikia.

“Ni kweli [mke wangu] alikuwa katika barabara ya Namanga, ambako alipishana kauli na askari wa usalama, nami nilifuatilia suala hili kwa undani sana. Ninachoweza kusema sitaki kuingia kwenye malumbano juu ya suala hili kwa kuwa limemalizika,” alisema.

Katika hatua nyingine, Balozi Mahiga alizungumzia picha iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha akiwa ameloa sehemu ya mbele ya suruali yake. Alisema kuwa hafahamu nia ya watu hao kusambaza picha hiyo ya kuudhi.

“Hata mimi sijui lengo lao nini kuisambaza ile picha, maana mimi niliiona kama ulivyoiona wewe,” Balozi Mahiga anakaririwa na Mtanzania..

IGP Mangu atoa masharti ya kumpandisha cheo trafiki aliyepambana na mke wa waziri
Sumaye aishangaa Serikali ya Magufuli, adai Mwenendo wake ni hatari