Wapiganaji wa kundi la Taliban wamelishilia jiji muhimu la Jalalabad nchini Afghanistan baada ya kuliteka kwa mtindo wa ‘kimyakimya’ bila mapigano yoyote.
Tukio hilo limekuwa hatua muhimu kwa kundi hilo kwani hadi sasa Serikali ya Afghanistan imebaki na jiji la Kabul pekee kama jiji muhimu.
Taliban wameshika jiji la Jalalabad mapema leo asubuhi ikiwa ni baada ya kulishika jiji muhimu zaidi la upande wa Kusini la Mazar-i-Sharif.
Kundi hilo limeweka kwenye mtandao wa kijamii picha inayowaonesha wakiwa ndani ya ofisi ya Gavana wa jiji la Jalalabad.
“Tuliamka asubuhi tukaona kuna bendera nyeupe jiji zima. Taliban waliingia kimyakimya, hakukuwa na mapigano ya aina yoyote,” Ahmad Wali, mkaazi wa jiji hilo anakaririwa na AFP.
Mbunge wa jimbo hilo, Abrarullah Murad aliiambia The Associated Press kuwa Taliban walilikamata jiji hilo bila mapigano baada ya viongozi kujadiliana na kukubaliana kusalimu amri, kwani mapigano yangeumiza raia na bado yasingeweza kuzuia.
Kundi hilo limeendelea kukamata majiji muhimu ya Afghanistan ikiwa siku chache tangu Marekani itangaze kumaliza oparesheni zake nchini humo. Rais Joseph Biden ametoa tamko rasmi kuwa baada ya miaka 20 ya mapigano nchini Afghanistan, haoni umuhimu wa majeshi ya Marekani kuendelea kupigana katika ardhi ya ugenini yenye vita ya wenyewe kwa wenyewe.
Rais Biden ameweka wazi kuwa Marekani iliingia Afghanistan kupambana na kundi lililotekeleza mashambulizi ya Septemba 11, 2001, kundi la Al-Qaeda. Amesema miaka 10 baadaye walifanikiwa kumuua Osama Bin Laden na kulidhoofisha sana kundi lake. Sasa kilichobaki kwa mujibu wa Rais ni Serikali ya Afghanistan kulinda ardhi yake.
Rais Biden ameitaja vita inayoendelea Afghanistan sasa kuwa ni vita ya wenyewe kwa wenyewe na haina uhusiano na mpango wa Marekani wa miaka 20 iliyopita. Amesema kuwa Marais wanne wamepitia katika vita hiyo, na sasa yeye akiwa ndiye wa nne hataruhusu kamwe imfikie Rais wa tano.
Kwa mujibu wa mkuu huyo wa taifa la Marekani, wametumia zaidi ya $1trilioni, kuwapa mafunzo wanajeshi zaidi ya 300,000 wa Afghanistan na kuwapa vitendea kazi. Pia, kuweka wanajeshi wake kwa maelfu katika ardhi ya Afghanistan, sasa anaona ni muda muafaka wa kuondoka na hatarudi nyuma.
Hata hivyo, amesema wamewapa angalizo Taliban kuwa wasiguse mali ya Marekani au watu ambao wana uhusiano na taifa hilo wakati wanajiandaa kuondoka; wakikiuka watakabiliwa na mashambulizi ya moja kwa moja kutoka kwa majeshi ya Marekani.