Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amewaagiza viongozi wote katika maeneo yanayonufaika na fedha za uwajibikaji – CSR, kuhakikishe wanazisimamia vizuri na kuzitambulisha kwenye Mabaraza ya Madiwani, ili waweze kuzipangia utaratibu wa matumizi kama ilivyokusudiwa.
Majaliwa ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Busega, Simon Songe Bungeni jijini Dodoma aliyetaka kujua ni nini mpango wa Serikali katika kuhakikisha fedha za CSR zinatumika kwa wakati pindi zinapofikishwa katika maeneo husika.
Amesema, fedha hizo za CSR zinapaswa kuingia kwenye mfuko wa mapato ya ndani ya kijiji au halmashauri, ili iweze kuratibiwa na kupangiwa miradi ya kutekeleza kulingana na mahitaji ya jamii husika.
“kutokana na miradi mbalimbali ya uwekezaji, fedha hii inapoingia inakuwa sehemu ya bajeti na ni lazima itumike na Serikali inazisimamia kupitia halmashauri zetu hivyo mzitambulishe kwenye mabaraza ya Madiwani,” amesema Waziri Mkuu Majaliwa.