Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), limewasilisha kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), maombi ya kupandisha bei ya huduma ya Umeme nchini kuanzia Aprili mosi mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa zilizowekwa kwenye tovuiti ya Ewura, Tanesco wamewasilisha maombi hayo kwa mujibu wa Sheria ya Umeme namba 131, inayoitaka Ewura kufanya mabadiliko ya bei zinazotozwa na mtoa huduma mara moja kila baada ya miaka mitatu.

Ewura imeeleza kuwa imepokea maombi hayo Jumatano wiki hii, na tayari imeanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau kuhusu maombi hayo ya Tanesco.

“Kwa mujibu wa kifungu Na. 19(2) (b) cha Sheria ya EWURA, Sura Na. 414, Mamlaka inaanzisha mchakato wa kupata maoni ya wadau ili kujua uhalali wa maombi ya nyongeza ya bei za huduma iliyoyapokea kutoka Tanesco,” imeeleza taarifa hiyo.

“Pendekezo la wastani wa badiliko la bei za umeme ni asilimia 1.1 kuanzia Aprili mosi 2016 na asilimia 7.9 kuanzia Januari mosi 2017,” imeongeza.

Maombi hayo ya Tanesco yanakinzana na agizo la Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, aliyeagiza Shirika hilo kwa kushirikiana na Ewura na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kuhakikisha inawasilisha kwake mapendekezo ya namna ya kushusha bei ya umeme nchini.

 

Vurugu zavunja uchaguzi wa Meya wa jiji la Dar, Polisi wawazima Ukawa
Video Mpya: Nay wa Mitego - Shika Adabu Yako