Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa Tanzania imeruhusu nchi 15 kupitia balozi zao kuleta waangalizi wa kimataifa kwenye uchaguzi mkuu.
Amesema kuwa baada ya balozi hizo kuwasilisha maombi na kufuata taratibu mataifa yao yatapaka kibali cha kuwa waangalizi katika uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika oktoba 28 mwaka huu.
Kabudi amesema hay leo Septemba 15,2020 jijini Dar es Salaam, wakati akifanya mazungumzo na Balozi wa Umoja wa Ulaya Balozi Manfred Fanti, ambapo amesema kuwa kwa mara ya kwanza uchaguzi huo unafanyika kwa kutumia fedha za ndani na sio wahisani kama miaka iliyopita.
Mbali na Balozi wa Ulaya Profesa Kabudi pia amekutana na Balozi wa Italia Roberto Mengoni, na Balozi wa Poland ambapo amekabidhi vitabu vya sheria ,kanuni na miongozo mbalimbali inayohusu masuala ya uchaguzi ili kuwapa fursa ya kufahamu jinsi uchaguzi unavyoendeshwa.
Kwa upande wake Balozi wa Umoja wa Ulaya Manfred Fanti amesema, ameridhishwa na namna kampeni zinazofanyika kwa uhuru na amani na sasa wanajiandaa na uangalizi wa uchaguzi huo.