Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt Hussein Ali Mwinyi akiwa katika siku ya mwisho ya ziara yake ya Qatar akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, alikutana na Waziri anayeshughulikia masuala ya Nishati wa Qatar, Mhandisi Saad bin Sherida Al Kaabi.
Katika mazungumzo hayo, walijadili juu ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Qatar kuhusiana na uchimbaji wa mafuta na gesi Zanzibar na mkutano huo ulilenga namna ambavyo nchi hizo mbili zinaweza kufanya kazi pamoja katika eneo hilo ambapo Dkt. Mwinyi alimfahamisha Waziri huyo wa Qatar kuhusu sera ya Zanzibar ya Uchumi wa Buluu na jinsi Qatar inaweza kuwa msaada katika suala la uchimbaji wa rasilimali hiyo.
Aidha, Dkt. Mwinyi amemwambia Waziri wa Nishati wa Qatar kutuma wataalamu wake Zanzibar ili kufanya kazi kwa pamoja na wataalamu wa Zanzibar kuchunguza uwezekano wa kuanza haraka uchimbaji wa rasilimali hizi na kusisitiza kuwa ushirikiano wa pamoja na ujuzi wa kitaalam kutoka Qatar unaweza kuchochea maendeleo na utekelezaji wa uchimbaji huo kwa ufanisi na kwa kasi.
Waziri wa Nishati wa Qatar, Mhandisi Saad bin Sherida Al Kaabi, alielezea kuwa nchi yake tayari ina uzoefu wa kufanya kazi na mataifa ya Afrika katika uchimbaji wa mafuta na gesi. Alikuwa wazi kuwa Qatar imekuwa ikisaidia nchi nyingi barani Afrika katika sekta hii na iko tayari kuendelea kufanya hivyo na Zanzibar.
Baadae, alikutana na Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Jassin bin Saif Ahmed ambapo katika mkutano huo, Dkt. Mwinyi alimuelezea Waziri huyo kuhusu mipango ya Zanzibar kuhusu mradi mkubwa wa ujenzi wa Bandari ya Mangapwani, ambayo itakuwa kituo kikuu cha kupakia na kupakua mizigo. Dk. Mwinyi alipendekeza kuwa Serikali ya Qatar inaweza kutoa msaada katika ujenzi wa bandari hiyo.
Hata hivyo, Waziri wa Uchukuzi wa Qatar, Jassin bin Saif Ahmed, alionyesha shauku kubwa kuhusu mradi huo, hasa baada ya kupewa taarifa kuwa eneo la ujenzi wa Bandari ya Mangapwani lina kina cha mita 18, ambacho ni kina kinachofaa kwa meli kubwa za mizigo.