Serikali imeridhia kutekeleza malengo endelevu 17, ikiwemo lengo linalohusu usawa wa kijinsia ifikapo mwaka 2030.

Hayo yamebainishwa na Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson wakati akifungua Kongamano la Taifa la Jinsia, jana Septemba 12, jijini Dodoma.

Amesema sambamba na hatua hiyo ya Serikali ambayo inaweka mazingira wezeshi kwa wanawake katika uchaguzi ujao, pia suala la uhamasishaji baina yao ni jambo muhimu.

Dkt. Tulia ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kongamano hilo, amesema suala la uhamasishaji ni sehemu ya ushindi kwa wanawake na kwamba anaamini bila hatua hiyo malengo yaliyokusudiwa hayatafanikiwa.

Awali, akizungumza katika kongamano hilo, Mbunge wa viti maalum (CCM) Mkoani Dodoma Bi. Fatma Toufiq, amesema mpango huo unatokana na marekebisho ya sheria ya mwaka 1977 iliyorejewa mwaka 2000-2004 wenye lengo la kuongeza ushiriki wa wanawake katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Katika tamko lao pamoja la muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali yanayotekeleza mradi endelevu wa usawa wa kijinsia kupitia muwakilishi wa Shirika la Sauti ya Wanawake Ukerewe, Mwenyekiti mwenza wa mashirika nane yanayoshughulika na mambo ya usawa Bi. Sophia Donard amesema mpango huo hautafanikiwa kwa kiwango kinachokusudiwa bila ushiriki wa wanaume.

Lengo la kongamano hilo ni kuimarisha ushirikiano kati ya watoa maamuzi na makundi ya wanawake, ili kuwawezesha wanawake na wasichana kushiriki katika ngazi mbalimbali za uongozi na maamuzi.

 

Video: Serikali yatoa sababu gharama za vipimo Muhimbili kuwa juu
LIVE: Yanayojiri Bungeni Dodoma leo Septemba 13, 2019