Serikali ya Tanzania imejipanga kuendelea kunufaika na fursa zinazotokana na Mtangamano wa Kikanda ili kuwawezesha watanzania kufaidika na uanachama wa Tanzania katika Jumuiya mbalimbali za kikanda.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Stergomena Tax wakati wa ufunguzi wa semina kuhusu nafasi ya Tanzania katika Mtangamano wa kikanda iliyotolewa na Wizara jijini Dodoma kwa Wajumbe kwa Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa lengo la kukuza uelewa.
Amesema, mtangamano wa kikanda ni dhana muhimu katika kukuza uchumi, kuimarisha uhusiano wa kisiasa, amani na usalama katika mataifa na kwamba Kamati hiyo ni miongoni mwa wadau muhimu wanaotakiwa kuwa na uelewa mkubwa kuhusu mtangamano wa kikanda ili kushirikiana na Wizara kueleza fursa na faida zake kwa wananchi.
Dkt. Tax ameongeza kuwa kwa Tanzania mtangamano wa kikanda ni sehemu ya utekelezaji wa Sera ya Mambo ya Nje hivyo uelewa wa pamoja kuhusu dhana hii hususan fursa, faida na changamoto na namna ya kuzitatua unahitajika ili kufikia malengo kusudiwa.
Tanzania ina mchango mkubwa katika Mtangamano wa kikanda na inategemewa ambapo pia imeendelea kunufaika na fursa mbalimbali zinazotokana na uanachama wake katika Jumuiya za Kikanda hususan, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
ikiwemo ajira, biashara, teknolojia, elimu na uwekezaji.
Awali akiwasilisha mada hiyo, Mkufunzi kutoka Chuo cha Diplomasia cha jijini Dar es Salaam, Bw. Charles Mtakwa amesema zipo faida nyingi kwa Tanzania kuwa mwanachama katika EAC na SADC ikiwemo ajira, biashara, elimu, teknolojia na uendelezaji miundombinu ya kikanda.