Waziri wa Madini na Maendeleo ya Migodi wa Zambia, Paul Kabuswe yupo nchini Tanzania kujifunza namna wachimbaji wadogo wanavyofanya shughuli za uchimbaji wa madini ya dhahabu, namna biashara ya madini ya dhahabu inavyofanyika kupitia masoko ya madini.
Akiwa na mwenyeji wake, Waziri wa Madini wa Tanzania, Doto Biteko jijini Dodoma, Kabuswe amesema usimamizi mzuri wa mfumo uliopo kwenye sekta ya madini nchini umewafanya kuja kujifunza namna wanavyosimamia sekta hiyo ili kunufaisha wananchi wao.
“Zambia inatarajia kufanya marekebisho ya Sera na Sheria zake za madini hivyo ujumbe huu umefika kwa jambo moja la kujifunza mfumo mzima na kupata mfano kwa Tanzania ni vyema sana kujifunza kwa nchi nyingine Afrika na duniani,” amesema Waziri Kabuswe.
Amesema, nchi ya Zambia na Tanzania zimekuwa na uhusiano na ushirikiano wa kipindi kirefu na wameshuhudia namna uchimbaji mdogo wa madini ulivyofanikiwa nchini hivyo, ujumbe huo umefika kujifunza na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kusimamia sekta ya madini.
“Sisi ni Serikali mpya tupo kwenye ofisi kwa takribani miezi kumi kwa hiyo tumeona tuje kujifunza kwa kuwa miongoni mwa vitu ambavyo Tanzania imefanya vyema ni usimamizi wa rasilimali za madini kwa wachimbaji wadogo,”amebainisha Waziri Kabuswe.
Amebainisha kuwa, ‘‘Tumeona hatunufaiki ipasavyo na sekta ya madini, tunataka watu wetu wapate ajira kwenye nafasi muhimu kupitia sekta hii, tunataka wananchi wanufaike ipasavyo ili vizazi vyetu vijavyo visikute mashimo tu, tunayo madini kama dhahabu, shaba, manganese tunataka madini haya yalete tija kwa Taifa.”
Awali, Waziri wa Madini Nchini, Doto Biteko amesema kiongozi huyo na ujumbe wake wapo nchini kujifunza usimamizi wa sekta ya madini hasa uchimbaji wa dhahabu unaofanywa na wachimbaji mdogo.
Amesema, mgeni wake Waziri Kabuswe atakwenda kwenye machimbo kuangalia namna wachimbaji wadogo wanavyotimiza majukumu yao, na kutembelea baadhi ya masoko ya madini yaliyopo nchin, huku akibainisha kuwa Zambia imeona upo umuhimu wa kuwaleta tena wataalam wake kuja kujifunza kwa kina.