Rais wa Marekani, Donald Trump amesema kuwa Korea Kaskazini ambayo imekuwa na uhasama na nchi yake kwa miongo kadhaa, ingekuwa kati ya mataifa yenye nguvu zaidi duniani kiuchumi.
Rais Trump ametumia ukaunti yake ya Twitter kuelezea mtazamo wake huo, akidai kuwa uwekezaji katika silaha za kinyuklia ndio sababu iliyolikwamisha taifa hilo.
“Mwenyekiti Kim [Jong Un], labda mtu bora kuliko mtu mwingine, bila silaha za nyuklia, nchi yake ingeweza kuwa moja kati ya nchi zenye nguvu zaidi ya kiuchumi duniani. Kwa sababu ya eneo la nchi yake na watu wake (pamoja na yeye), ina nafasi kubwa ya kukua haraka kiuchumi kuliko taifa lingine lolote,” tafsiri isiyo rasmi ya Tweet ya Trump.
Ameandika hayo ikiwa ni saa moja tu tangu Waziri wa Mambo ya ndani wa Marekani, Mike Pompeo aeleze kuwa Korea Kaskazini bado ni tishio kwa silaha za nyuklia.
Ripoti hiyo haikuchukuliwa kwa mtazamo hasi na Rais Trump ambaye anatarajia kufanya mkutano wa pili na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, Februari 27-28 mwaka huu nchini Vietnam.
Trump amesema kuwa hatawaharakisha Korea Kaskazini kuachana kabisa na silaha za kinyuklia bali hata kuacha kufanya majaribio tu kwa kipindi hicho ni hatua nzuri kwake.
“Wote tunategemea kutakuwa na muendelezo wa mazungumzo tuliyoyafanya katika mkutano wa kwanza. Sitaki kumharakisha mtu yeyote. Ili mradi hivi sasa hakuna majaribio ya nyuklia, sisi tuna furaha,” alitweet.
Mkutano wa kwanza wa Kim na Trump nchini Singapole ulikuwa wa kihistoria, kwakuwa Marais wa kwanza wa nchi hizo walioko madarakani kukutana. Mkutano wa pili wa Vietnam utakuwa wa kihistoria pia.