Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muugano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa maabara ya afya ya jamii kwenye Hospitali ya Taifa ya Magonjwa Ambukizi ya Kibong’oto na kusema kuwa amefarijika kuona lengo la Rais Dkt. John Magufuli katika sekta ya afya likitekelezwa.

Amesema Rais Dkt. Magufuli anataka kuona watanzania wote wanapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya karibu na makazi yao, hivyo wananchi hawana budi kuendelea kumuamini na kushirikiana na Serikali yao.

“Rais wetu Dkt. Magufuli ana nia thabiti ya kuwahudumia Watanzania wote walioko katika maeneo yote nchini. Wananchi wote wanapata huduma sawa bila ya ubaguzi wa aina yoyote, hivyo endeleeni kuiamini Serikali yenu.”

Majaliwa ameyasema hayo alipotembelea hospitali hiyo ya Kibong’oto iliyoko kwenye mtaa wa Mae kata ya Ivaeny wilayani Siha akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Kilimanjaro.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema wilaya hiyo imepewa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa hospitali ya wilaya na kuhusu upatikanaji wa dawa kwenye vituo vya kutolea huduma za afya kwa sasa umefikia asilimia 95.

Awali, Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali ya Kibong’oto Dkt. Riziki Kisonga alisema ujenzi wa jengo hilo utafanyika kwa awamu tatu, awamu ya kwanza itagharimu sh. bilioni 2.183 na ilianza Septemba 2018 na inatarajiwa kukamilika Julai mwaka huu.

Dkt. Kisonga alisema jengo hilo ni la ghorofa tatu zenye pande mbili pacha, upande wa kwanza ni kwa ajili ya kazi za maabara kwa uchunguzi wa vimelea hatari na hatarishi sana na virusi vinavyosababisha milipuko ya magonjwa kama marburg, ebola, chikungunya na dengue.

“Umuhimu wa maabara hii ni kusaidia kutoa huduma za uchunguzi wa magonjwa ambukizi yakiwemo ya kifua kikuu na magonjwa mengine yasiyoambukiza katika ubora unaotambulika kimataifa.”

Dkt. Kisonga alisema maabara iliyopo hospitalini hapo kwa sasa imepata ithibati ya kimataifa ya kufanya vipimo vya ngazi ya daraja la pili, hivyo baada ya kukamilisha ujenzi huo watakuwa na uwezo wa kufanya vipimo vya ngazi ya daraja la tatu.

R Kelly azidi kusota lupango, akosa pesa ya dhamana
Trump adai Korea Kaskazini ingekuwa taifa lenye nguvu zaidi duniani