Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Innocent Bashungwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa Kagera, Albert John Chalamila kuunda Tume maalum itakayopokea malalamiko ya ardhi yaliyokithiri katika Halmashauri ya wilaya ya Karagwe, Mkoani Kagera.
Ametoa agizo hilo aliposhiriki kikao cha Halmashauri kuu ya Chama Cha Mapinduzi wilaya Karagwe na kupokea malalamiko ya kuibuka na kukithiri kwa migogoro sugu ya ardhi ndani ya wilaya ya Karagwe.
Amesema Tume hiyo maalum itafanya kazi ya kufuatilia kwa undani migogoro sugu na inayoendelea kuibuka ndani ya mkoa wa Kagera ambayo inachangia uvunjifu wa amani na kuleta umasikini kwa wananchi.
Aidha, Bashungwa amepokea changamoto kuhusu vijana wasiokuwa na Vitambulisho vya NIDA kutopewa Mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri ambapo Bashungwa amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo ambayo ipo katika mfumo Mpya wa utoaji wa Mikopo katika Halmashauri.